Free Web Hosting Provider - Web Hosting - E-commerce - High Speed Internet - Free Web Page
Search the Web

Trninity Band






  


TRINITY SINGERS!


TRINITY SINGERS Dar es Salaam, Tanzania

Kundi la Trinity Singers lilianzishwa mwezi wa nane 2004 likiwa na jumla ya watu wanne; Abdon Mhando, Elizabeth Mhando, Suzan Mhando ambao walikua waimbaji na Ivan Chiduo kama kiongozi (Meneja wa Kundi). Tangu wakati huo kundi hili limekuwa na kufikisha jumla ya watu watano. Waanzilishi wa kundi hili walikuwa ni Ivan, Abdon na Eliza, waliojiunga baadae walikuwa ni Joyce, Suzan na Kenneth.  Hata hivyo, Joyce ndiye mdogo zaidi katika kundi hili la Trinity Singers. 

 

Joyce alianza kuimba katika umri mdogo pale alipokuwa katika shule ya msingi. Alipofikisha umri wa miaka kumi tayari alikuwa amefanikiwa kuanza kuimba katika kwaya ya kanisa alilokuwa akisali wakati huo. Joyce anasema yeye anapenda kuimba lakini anafurahia zaidi inapofikia hatua ya kuucheza muziki wenyewe, "napenda sana kucheza muziki, na kumchezea Bwana ndicho ninachopenda kufanya" ananukuriwa akijielezea. 

 

Kwavile alizaliwa kwenye familia ya wanamuziki, Kenneth alijikuta katika ulimwengu wa muziki akiwa na miaka 9 tu! Tangu umri huo mdogo amekuwa akijishughulisha na upigaji wa magitaa na vinanda katika kwaya za kanisa. Amekuwa akifanya hivyo mpaka pale alipojiunga na kundi la Trinity Singers, ndipo alipogundua kuwa anaweza fanya jambo lingine zaidi ya upigaji wa vyombo, anaweza kuimba pia, " Ken anaweza kufanya mambo mengi" anakaririwa Ivan akielezea, Anaweza kuimba, kupiga magitaa na vinanda, pia aweza kutunga nyimbo na kufanya upangiliaji wa muziki. 

 

Eliza ambaye pia hujulikana kwa jina la 'Liz', ni mmoja ya watu waliozaliwa na kipaji halisi cha uimbaji. Ameanza kuimba miaka kumi na sita iliyopita wakati akiwa shule ya msingi. Pia ameshirikishwa kama muimbaji msaidizi na wanamuziki mbalimbali wa nyimbo za injili walipokuwa wakirekodi nyimbo zao. ' Napenda kuimba na zaidi ya yote napenda kuona uimbaji wangu ukileta mabadiliko ndani ya maisha ya watu' naweza imba kwa kuburudisha lakini kusudio langu ni kuimba na kuleta mabadiliko ndani ya maisha ya mwanadamu' hivyo anavyosema. 

 Suzana naye pia alianza kuimba akiwa na miaka 9. Walikuwa ni walimu wake wa shule ya msingi ambao waligundua kipaji chake cha uimbaji. Baada ya muda alianza kuimba katika kwaya ya kanisa. "Sikuwa hasa nafahamu nini nafanya wakati ule" anaeleza Suzana na kuendelea, "walikuwa wakinisimamisha kwenye kiti wakati ninapotakiwa kuimba, maana nilikuwa mdogo, sikujua nilichokuwa nafanya! Lakini ni tofauti sana sasa, maana wakati huu ninaimba nikiwa na makusudio maalumu."    Abdon pia alianza kuimba katika kwaya ya kanisa miaka kadhaa iliyopita, na baadae katika kundi la kifamilia la Trinity, alishiriki kwenye album ya Trinity ya kwanza "Amani Africa", hata hivyo kwa sasa hayupo tena kwenye safu ya uimbaji kutokana na majukumu ya kikazi yaliyo juu ya iwezo wake, yeye amebaki kama mshauri tu. 

Ivan yeye pia amekuwa akijihusisha na mambo ya muziki tangu alipokuwa mdogo. Yeye ni mtunzi na pia anapenda sana kujishughulisha na upangaji wa muziki. Ivan ni mwanzilishi wa kundi la Trinity Singers.  Zaidi ya wahusika watano wanaounda kundi la Trinity Singers, pia kuna umoja ambao tunapenda kuuita ' Familia ya Trinity Singers'. Huu ni mjumuiko wa watu ambao huwa tunakuwa nao mara nyingi na kufanya nao kazi mara kwa mara. Wao ni sehemu ya huduma yetu, wanatusaidia katika mambo mengi. Tunamshukuru Mungu sana kwa wao kufanyika sehemu ya huduma yetu. Tunapozungumzia familia ya Trinity hatutaweza kuacha kutaja majina yafuatayo; Barabara, Furaha, Rachel,Pendo William na Florah Njama.  Ni zaidi ya miaka miwili sasa tangu kuanzishwa kwa kundi la Trinity Singers. Katika muda wote huo haikuwa rahisi, tumepambana na magumu mengi, lakini katika yote tumemuona Mungu akiwa upande wetu. Imeweza kuwa 'safari salama' sababu tu Bwana amekuwa nasi. Nia na hamu ya miyoyo yetu ni kuyagusa maisha ya watu kupitia muziki wetu. Tunatamani watu waje kwa Yesu kupitia uimbaji wetu, waliovunjika moyo wakapate kupona, na wale waliokata tamaa, wakapate kutiwa moyo kupitia huduma yetu ya uimbaji.  

 'Jiandae' ni CD yetu ya pili baada ya ile iliyotolewa mwaka 2005 na kupewa jina la 'Amani Afrika'. Nyimbo zote zilizomo katika albam hii ya Jiandae zimerekodiwa katika Studio za FM zilizopo jijini Dar-es-salaam. Jiandae pamoja na kubeba jina la CD hii mpya pia ni jina la wimbo. Tumependa kutumia neno 'Jiandae' maana sisi kama wakristo na watu wa Mungu wote tunapasawa kuwa tayari kwa maana ujio wa Kristo Yesu ukaribu sana. Ni maombi yetu mbele za Mungu kwamba nyimbo hizi zitavuka mipaka ya tamaduni na hata lugha na kugusa moyo wa kila mmoja atakayekwenda kuzisikiliza.   AKSANTENI
 

ELIZABETH

Kwa unyenyekevu napenda kumshukuru Mungu wetu, yeye aliye muumbaji wetu na mtoaji wa vipaji. Mungu uko pamoja nasi nyakati zote na kutuweka katika mpango na makusudio yako kwaajili ya utukufu wako. Tunayo kila sababu ya kukutukuza na kusema asante Mungu. Kwenu nyote mlio mashabiki wetu na watu mnaotusaidia katika mambo mbalimbali, tunapenda kuwashukuru kwa kuwa nasi wakati wote na kwa imani yenu kubwa kwetu.  Tunawashukuru wachungaji wetu wote kwa kututunza kiroho.  Mama na Baba, kazi yenu ya kunitia moyo na imani yenu kwangu vimenifanya niwe jasiri zaidi katika kile nikifanyacho, ninawapenda sana!  Kwa menaja wetu Ivan, asante kwa kusaidia ukuwaji wa kipaji changu.  Kaka Abdon, asante kwa ushauri wako na kwa kuwa nasi nyakati zote.  Furaha na Barabara, maneno hayatoshi kuelezea vyema shukrani zangu kwenu.  Wafanyakazi wote wa studio za FM, asanteni kwa kazi kubwa mliyofanya.  Mwisho kwa wezangu wote ndani ya Trinity Singers, asanteni sana kwa kusafiri safari hii pamoja nami, sitosahau upendo wenu kwangu.    

 

KENETH

Sifa na utukufu ni kwako Mungu uliyetuwezesha kumaliza kazi ya kutengeneza kazi hii ya 'Jiandae'. Haikuwa rahisi lakini Mungu umetuwezesha. Shukrani za dhati kwa familia zetu kwa kututia moyo na kutusaidia. Mmetusaidia kwa hali na kwa kiroho, Mungu awabariki sana. Kwenu Barabara na Furaha, asante kwa kazi kubwa mliyoifanya, Trinity singers isingefika ilipoweza kufika bila mchango wenu. Wote pale FM, tumefurahi sana kufanya kazi nanyi.

JOYCE

Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kumtumikia kupitia huduma hii ya muziki. Kwa yale yote nifanyayo, sifa na utukufu vimwendee Mungu. Najua siwezi kusimama peke yangu Bwana bila wewe, na katika kuandaa kazi hii ya Jiandae nimeendelea kukuona Mungu.

SUZAN

Kwanza kabisa napenda kumshukuru aliye juu kwa kunipa kipaji cha kuweza kuimba na kuniwezesha kuielezea imani yangu kwa dunia nzima. Namshukuru mama yangu kwa kunisaidia nyakati zote, mama wewe ni bora zaidi! Kaka yangu Joakim, ninajua unapenda na kunitakia mema, ninakila sababu ya kukushukuru.  Kila mmoja ndani ya Trinity Singers, 'tuko pamoja' asanteni kwa ushauri wenu na masada wenu.  Kwa mashabiki wetu, tunawapenda sana, tunawaomba muendelee kutusaidia na kamwe hatutawaangusha.

 

ABDON

Asante baba muweza wa yote kwa ajili ya baraka ambazo unatupa. Kwa moyo wangu naamini kuwa Mungu utakwenda kuibariki kazi ya yetu, tumekua tukikuona sana katika kazi yetu, umekua msaada wetu sana, tunakushukuru. Kwenu baba na mama Mr and Mrs Billy Mhando, Mr & Mrs. Chiduo, familia ya Beatus Msisi na Dr. Williamu Mwegoha asanteni kwa kuwa nasi nyakati zote za huduma yetu, Mungu atawalipa kwa msaada wenu usiopimika kwa fikra za kibinadamu tu, mmeifania Trinity mambo mengi sana. Shukrani pia kwa watu wa Mungu, wapenzi wa Trinity na watanzania wote wote mnaosikiliza kazi zetu. Mwisho, kwa watu wote popote pale Duniani ambapo umenunua kazi zetu.

IVAN

Asante baba wa mbinguni kwa ajili ya baraka ambazo unatupa. Asante kwa kuwa Bwana na Mwokozi wetu. Asante Mungu kwa kuifikisha Trinity Singers hapa ilipo. Tunajua wazi kuwa bila wewe Mungu tusingeweza chochote. Kwa moyo wangu naamini na kwa mdomo wangu nakiri na kutangaza kuwa Mungu utakwenda kuibariki kazi ya yetu. Kwenu Andrew, Billy Mhando, Mr & Mrs. Chiduo, asante kwa kuwa nasi nyakati zote, Mungu atawalipa kwa msaada wenu mkubwa mnaotupatia. Redio zote Tanzania na kwingineko, nawashukuru sana kwa kupiga muziki wetu. William Mwegoha, asante kwa kazi kubwa uliyoifanya katika kutengeneza 'Jiandae'. Kwenu marafiki na mashabiki wetu wote, asanteni kwa msaada wenu na kuwa pamoja nasi. Mungu awabariki wote!

 

 

Abdon's Website